Sunday, September 2, 2012

MUENDELEZO WA SOMO LA MADHEHEBU

Assalaam Alaykum!Naam tuendelee na kufahamishana mawili matatu kuhusiana Uislaam!Baada ya kuona makemeo ya Allah juu ya kuigawanya Dini na kuwa Makundi Makundi(Madhehebu) kwa kutuonesha kuwa kufanya hivyo ni Ukafiri na ni Ushirikina!Tuone basi ni kipi hicho CHANZO CHA MADHEHEBU KATIKA UISLAAM!Jambo ambalo ndio Mada ya Siku yetu ya leo!
Ndugu zangu,Njama za kuugawa Uislaam hazikuanza jana wala juzi,bali tangia Enzi za Bwana Mtume Muhammad(s.a.w).Jambo hilo la kuigawa Dini lilikuwa likifanyika kila mara anapoletwa Nabii/Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa lengo la wale wenye kutawala waendelee kuwatawala Watu ambao wakishaujua Ukweli kuhusiana na Maisha yao kwa ujumla hawatokuwa na njia nyingine ya kuwatawala.
Jambo hilo ililazimu wale wanaotaka kuendelea kutawala,wapambane na Manabii wa Mwenyezi Mungu kwa kuiviza na kuifahamisha vingine ile Haki iliyokwisha kuja kwa lengo lao hilo.Sitaki tuzame sana huko lisije Somo letu likawa refu sana hata Msomaji akashindwa kuzingatia!Turudi sasa katika kuangalia hizo njama zilizokuwa zikifanyika wakati wa Uhai wa Mtume(s.a.w) ili kuwagawa Watu!
Kitu cha Mwanzo walichofanya ni kuwaelekeza Watu na kuwapa mafunzo kinyume cha yale aliyokuwa akifundisha yeye Mtume,na hayo yalifanywa na wale Wanafiki waliokuwa wakijifanya kuwa ni Wanafunzi watiifu wa Mtume hali ya kuwa ni waongo!Hayo Mtume hakuwa akiyajua mpaka alipozinduliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe! "NA WANASEMA TUMETII,NA WANAPOTOKA KWAKO KUNDI MOJA MIONGONI MWAO HUPANGA NJAMA USIKU KINYUME CHA YALE UNAYOYASEMA..." (Sura ya 4 Aya ya 81).
Hawa walikuwa pamoja na Mtume!Wanasikiliza Aya za Mwenyezi Mungu mbele ya Mtume(s.a.w) mwenyewe kisha kumbe wanakuwa hawajaridhika na yale waliyofundishwa na Mtume,na kuamua kukaa vikao vya mapinduzi usiku kupindua yale alowafundisha Mtume!
Wafanya mapinduzi wa kabla ya Mtume walikuwa wakiyaingilia moja kwa moja yale Mafundisho ya Kitabu husika na kuyachakachua!ndivyo ilivyofanywa Taurati,Zaburi na Injili!lakini wafanya mapinduzi hawa wa zama za Mtume Muhammad(s.a.w) walikumbana na mkwamo,pale walipokumbana na Ahadi ya Mwenyezi Mungu kwamba "HAKIKA SISI NDIO TULIOUTEREMSHA UKUMBUSHO(QUR'AN) NA HAKIKA SISI NDIO TUTAKAOULINDA"(Sura ya 15 Aya ya 9)
Kwahiyo zoezi la kutia mafundisho yao ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili wapate kuwagawa Watu na kuendelea kuwatawala,likagonga mwamba!hata hivyo hawakukata tamaa,wakaona ni bora wamvae Mtume mwenyewe "NA WANAPOSOMEWA AYA ZETU ZILIZO WAZIWAZI,WALE WASIOTARAJI KUKUTANA NASI HUSEMA:LETE QUR'AN ISIYOKUWA HII AU IBADILISHE!SEMA:HAINIFALII MIMI KUIBADILISHA KWA ITAKAVYO NAFSI YANGU.MIMI SIFUATI ILA NINAYOFUNULIWA. HAKIKA MIMI NAOGOPA IKIWA NITAMUASI MOLA WANGU,ADHABU ILIYO KUU"(Sura ya 10 Aya ya 15).
kwa hiyo Jaribio lingine likakwama!Ndio ikawabidi sasa waingie kazini wenyewe kila Mtume anapofundisha hivi wao hutunga mengine ili kuwadanganya Watu na kuwatoa kwenye mstari ili waendeleze mambo yao waliyokuwa nayo kabla ya Mtume Muhammad kupewa Utume!Mwenyezi Mungu anatupa habari kwamba hali hiyo ya kumbadilishia maneno illikuwa ikimhuzunisha sana Mtume,hali iliyomlazimu Mwenyezi Mungu amtulize Mtume wake kwa kumwambia "EWE MTUME!WASIKUHUZUNISHE WALE WAFANYAO HARAKA KUKUFURU,MIONGONI MWA WANAOSEMA KWA VINYWA VYAO:TUMEAMINI NA HALI NYOYO ZAO HAZIJAAMINI,NA MIONGONI MWA MAYAHUDI,WANAOKUSIKILIZA ILI WAKASEME UWONGO,WANAOKUSIKILIZA KWA AJILI YA WATU WENGINE WASIOKUFIKIA.HUBADILISHA MANENO KUTOKA MAUDHUI YAKE..."(Sura ya 5 Aya ya 41)
Hiyo ndio kazi waliokuwa wakiifanya baadhi ya Wanafiki miongoni mwa Maswahaba wa Mtume wakishirikiana na Mayahudi,kutunga Maneno tofauti na alivyofundisha Mtume mwenyewe kama alivyoteremshiwa na Mola wake!Je Maswahaba hawa wazusi tutawajuaje hali ya kuwa Mtume Mwenyewe hakuwa akiwajua!"NA KATIKA MABEDUI WALIO PEMBEZONI MWENU KUNA WANAAFIKI,NA KATIKA WENYEJI WA MADINA PIA KUNA WALIOBOBEA KATIKA UNAAFIKI,WEWE HUWAJUI.SISI TUNAWAJUA.TUTAWAADHIBU MARA MBILI KISHA WATARUDISHWA KATIKA ADHABU KUBWA"(Sura ya 9 Aya ya 101).
Alaa kumbe miongoni mwa Maswahaba wa Mtume walikuwa ni Wanaafiki!halafu mbaya zaidi hata Mtume mwenyewe hakuwa akiwafahamu kwa Majina yao!Je sisi tutawajuaje toba Yaa Rabbi!
Mwenyezi Mungu alimtajia Mtume na Waislaam kwa ujumla,Sifa za wale Maswahaba wanafiki waliokuwa wakishirikiana na Makafiri ili kuwagawa Waislaam na wawe makundi makundi ili Ukafiri uendelee kutawala Duniani.Moja ya Sifa zao ni hii "LAU WANGELITOKA NANYI WASINGELIKUZIDISHIENI ILA MACHAFUKO,NA WANGELIKWENDA HUKU NA HUKO KATI YENU ILI KUKUTILIENI FITNA,NA MIONGONI MWENU WAPO WANAOWASIKILIZA SANA.NA MWENYEZI MUNGU ANAWAJUA MADHALIMU.TANGU ZAMANI WALITAKA KUKUTILIENI FITNA,NA WAKAKUPINDULIA MAMBO CHINI JUU,MPAKA IKAJA HAKI NA IKADHIHIRIKA AMRI YA MWENYEZI MUNGU NA HALI WAMECHUKIA"(Sura ya 9 Aya ya 47-48).Naam,ukianzia Aya za nyuma yake utaona namna Wanaafiki hao walivyokuwa wakihimizwa kwenda kuipigania Dini ya Mwenyezi Mungu nao wakijitia uzito kwenda,lakini kumbe ilikuwa kheri vilevile kwani hawana ambalo wangefanya huko Vitani ila kuitia chokochoko na fitna na kuna hatari ya kuwa wangegawa makundi kwa wengi wao walikuwa wakiwasikiliza sana wao wanaafiki kuliko Mtume!Na tayari walishampindulia mambo chini juu!Kwa kuingiza Mafundisho yao ya uwongo na kusema kuwa Mtume ndiye aliyesema hayo ili kufanikisha mambo yao!kivipi?
"NA WAPO BAADHI YAO WANAOPINDUA NDIMI ZAO KUKISINGIZIA KITABU ILI MDHANIE KUWA HAYO YANATOKA KWENYE KITABU,NA WALA HAYATOKI KATIKA KITABU.NA HUSEMA HAYA YAMETOKA KWA MWENYEZI MUNGU NA HALI HAYATOKI KWA MWENYEZI MUNGU,NA WANAMSINGIZIA MWENYEZI MUNGU UWONGO NA HALI WANAJUA!"(Sura ya 3 Aya ya 78)
Ndugu zangu,kumbukeni kuwa mambo hayo yalikuwa yanafanywa hali ya kuwa Mtume mwenyewe yu hai!Sikwambii alipokuja kufa!Yaani Watu wanatunga mafundisho ya uwongo ili yadhaniwe kuwa nayo ni Mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa lengo la kuwagawa Waislaam!kivipi?Kwa kutunga Mafundisho juu ya jambo moja kwa namna tofauti!Utaambiwa kwamba Mtume Muhammad(s.a.w) alifanya hivi au alitenda hivi!Fundisho ambalo litakuwa tofauti na fundisho lingine ambalo nalo atakuwa amesema au kutenda tofauti!ambalo nalo litatofautiana na lingine tena,katika tukio moja!au kikao kimoja!au mazingira mamoja!na cha ajabu hayo yote yanaweza kuwa kinyume kabisa na Kitabu kilivyoagiza!
Je ni vipi Mafundisho hayo yakaja kuwagawa Waislaam baada ya Mtume kufariki na kuwa katika hali tuionaya hivi sasa!TOA CHOCHOTE UNACHOKIFAHAMU,NA SOMO LITAENDELEA INSHAALLAH!......

SOMO LA MUENDELEZO WA MADHEHEBU

Assalaam Alaykum, Kumbukeni kuwa huu ni Uwanja mpana  unaruhusiwa kutoa maoni yako kwa namna ulivyojaaliwa ili mradi usimtukane Mtu wala kumdhalilisha!Ndugu zangu tutumie Akili na Fikra zetu,laa sivyo tutaenda kuhukumiwa kwa hilo!ALLAH anasema "NA KWA HAKIKA TUTAWAINGIZA JAHANNAM WENGI KATIKA MAJINI NA WATU.WANA MIOYO LAKINI HAWAFAHAMII KWAYO,NA WANA MACHO LAKINI HAWAONI KWAYO,NA WANA MASIKIO
LAKINI HAWASIKII KWAYO.HAO NI KAMA WANYAMA BALI WAO WAMEPOTEA ZAIDI.HAO NDIO WALIOGHAFILIKA"(Sura ya 7 Aya ya 179).
Akasema tena kuwa "HIKI (QUR'AN) NI KITABU TULICHOKITEREMSHA KWAKO ILI ZIZINGATIWE AYA ZAKE NA ILI WAKUMBUKE WENYE AKILI"(Sura ya 38 Aya ya 29).Na namalizia kwa kauli yake kuwa "......NA(MWENYEZI MUNGU) HUJAALIA UCHAFU KWA WALE WASIOTUMIA AKILI"(Sura ya 10 Aya ya 100).Aya zote hizo zinaonesha umuhimu wa utumiaji wa Akili na Fikra zetu katika kuyaendea mambo ya msingi,kwani ndicho kitu kinachomtofautisha Mwanaadamu na Wanyama wengine!Haiwezekani wakati wa Usiku Mtu akwambie kuwa huu ni Mchana nawe ukubaliane nae pasi na kufikiri!
Lakini vilevile,nilitoa Dondoo za udadisi ambazo zingemsaidia Mchangiaji katika kutoa maoni yake!Kwamba ikiwa Muongozo umekemea vikali juu ya Madhehebu(Makundi) na kuiorodhesha kuwa ni Ukafiri na Ushirikina,na ikiwa Mtume(s.a.w) hakuacha hali ya Umakundi(Madhehebu) ndani ya Uislaam!Je nini kilichosababisha hali hii ya umakundi ndani ya Uislaam?
Dodoso lingine likasema,Je hali hii ya Umakundi(Madhehebu) ndani ya Uislaam inaweza kuondoka na Dini kurudi kama wakati wa Enzi za Mtume(s.a.w)?
Somo litaendelea inshaallah....!

MADHEHEBU KATIKA UISLAAM NI USHIRIKINA NA NI UKAFIRI!


Assalaam Alaykum nyote!ndugu zangu hebu leo tuzungumze kuhusu hili!natanguliza kuomba radhi kwa lugha ngumu ntakayotumia,si kwa nia mbaya bali ni katika namna ya ufikishaji kwani tukiendelea kupambapambana kinafiki tutakuwa hatufiki!Sote tunafahamu kuwa Mgonjwa kama kupona kwake tiba yake ni kuchomwa sindano,japo ataumia ni lazima achomwe ili kupata uzima wake kama kweli tunampenda!
Madhehebu ni wingi wa neno Dhehebu ambalo maana yake ni Kundi la jamii ya watu wenye kufuata mwenendo na mrengo wa namna fulani iliyotofauti na wengine.
Uislaam ni Dini yenye Mfumo maalum ulioelekezwa na Muumba mwenyewe,Mfumo ambao alimpa Mtume wetu Muhammad(s.a.w) ili naye awafundishe watu.Sote tunafahamu kuwa Mtume(s.a.w) mpaka anafariki Dunia hakuacha ndani ya Uislaam Makundi(Madhehebu) katika jamii ya Waislaam.Mtume na wote waliomfuata walikuwa na mwendo wa namna moja,na wote waliokuwa wakiingia katika Uislaam aliokuwa akiuhuisha Mtume(s.a.w) walilazimika kushika mwendo uleule aliokuwa akiufundisha Mtume,NI UPI HUO?
Ni UMOJA wa kila Jambo katika Dini!Mwenyezi Mungu ni Mmoja(ALLAH),Mtume wetu ni Mmoja(Muhammad),Kitabu chetu ni kimoja(Qur'an),Dini yetu ni moja(uislaam).
Mtume(s.a.w) aliwaambia Waislaam "ENYI MLIOAMINI MUOGOPENI MWENYEZI MUNGU UKWELI WA KUMUOGOPA,WALA MSIFE ISIPOKUWA NI WAISLAAM.NA SHIKAMANENI PAMOJA KATIKA DINI YA MWENYEZI MUNGU NA WALA MSIGAWANYIKE!NA KUMBUKENI NEEMA ZA MWENYEZI MUNGU JUU YENU,PINDI MLIPOKUWA MAADUI BASI AKAZIUNGANISHA NYOYO ZENU NA MKAWA NDUGU KWA NEEMA YAKE(QUR'AN).NA MLIKUWA KATIKA UKINGO WA SHIMO LA MOTO BASI AKAKUOKOENI NALO.NAMNA HIVYO MWENYEZI MUNGU ANAKUBAINISHIENI AYA ZAKE ILI MPATE KUONGOKA!"(Qur'an 3:102-103)
Kwa hiyo Mtume alikuwa akilingania Umoja baina ya Waislaam wenye utaratibu mmoja,ambapo Mwenyezi Mungu alimtaka Mtume awakumbushe Historia yao waliokuwa Waislaam kuwa wamekuwa wamoja,ndugu badala ya hali ya utengano na uadui waliokuwa nao kabla ya kuwa Waislaam.Kwahiyo Uislaam ulikuwa ni mmoja,kundi moja-Kundi la Mwenyezi Mungu(Qur'an 58:22) na ni marufuku kuanzisha kundi ndani ya kundi moja la Uislaam!Bali kulikuwa na kundi lingine ambalo ni kundi la Shetani ambalo lilikuwa ni dhidi ya Waislaam.
Mara fulani kule Madina Wanafiki walijaribu kuanzisha Msikiti na wakamuomba Mtume aende kuuzindua.Mtume(s.a.w) kwa kuwa hakuwa akijua Ghaibu(Siri) aliwakubalia,lakini Allah mjuzi wa Ghaibu alimkataza Mtume wake asiende kuuzindua Msikiti huo kwa kuwa waanzilishi wake hawakuwa na lengo zuri katika kuuanzisha Msikiti huo "NA WALE WALIOTENGENEZA MSIKITI KWA AJILI YA KULETA MADHARA NA UPINZANI NA KUWAGAWA WAUMINI,NA KUWA SEHEMU YA KUJIFICHIA YA WALE WALIOMPIGA VITA MWENYEZI MUNGU NA MTUME WAKE ZAMANI......"(Qur'an 9:107).
Ndio kusema kuwa hao walikuwa ni wanafiki ambao Mwenyezi Mungu aliwaumbua!Kumbe miongoni mwa malengo yao ni kuwagawa Waumini!wasiwe kitu kimoja kwa manufaa yao binafsi kinyume na agizo la Mwenyezi Mungu la kuwataka Waislaam wawe ni kitu kimoja,kundi moja lisilo na mpasuko wala mgawanyiko!Mtume akaambiwa "USISIMAME KAMWE NDANI YA MSIKITI HUO..."(9:108)
Ndugu zangu njama za kuwagawa Waislaam zilendelea na kufanyiwa juhudi kubwa tangu enzi za Uhai wa Bwana Mtume Muhammad(s.a.w).Mtume aliwaasa Waislaam kwa kuwaambia hali akiwaonya "WALA MSIWE KAMA WALE WALIOGAWANYIKA NA KUTOFAUTIANA,BAADA YA KUFIKIWA NA UBAINIFU.NA HAO NDIO WATAKAOPATA ADHABU KUBWA KABISA"(Qur'an 3:105).Kumbe tulishonywa kuwa "Wala tusiwe kama wale!"Ina maana walikuwepo watu walikuwa wameigawa Dini yao na wakatofautiana ndani yake!NI KINA NANI HAO?
Hao si wengine bali ni wale waliopewa Uislaam zamani kisha wakauharibu kwa kuugawa makundi makundi na kila kundi likawa linajiona liko sawa.Wana wa Israel walipewa Uislaam kwenye Taurati kupitia Nabii Musa(a.s),wakaugawa Uislaam wao na ukawa Uyahudi,ambao nao uligawika katika makundi(Madhehebu) ya Uzayuni,Uothordox,Usquirs n.k.
Baadae wakapewa Injili kupitia Nabii Isa(a.s),wakauharibu Uislaam wao na waukaufanya kuwa ni Ukristo,ambao nao uligawika katika makundi(Madhehebu) ya Roman Catholic,Lutheran,Anglican n.k.
Sasa Waislaam walitakiwa wasiwe kama hao,wakati huo wao walikuwa ni kundi moja!wakaonywa tena "NYENYEKEENI KWAKE NA MUMUOGOPE NA SIMAMISHENI SWALA,WALA MSIWE MIONGONI MWA WASHIRIKINA.AMBAO WAMEIGAWA DINI YAO NA WAKAWA MAKUNDI MAKUNDI,KILA KUNDI LINAFURAHIA WALIYONAYO"(30:31-32).
Tunapata hitimisho kuwa kumbe Uyahudi na Ukristo ni Ushirikina kwa kuigawa Dini Makundi Makundi(Madhehebu).Tena Allah akaonya kwa mara nyingine kuwa "NA HAWATOKUWA RADHI NAWE MAYAHUDI NA WAKRISTO MPAKA UFUATE MILA YAO.SEMA HAKIKA MUONGOZO WA MWENYEZI MUNGU NDIO MUONGOZO HASWA,NA KAMA UTAFUATA MATAMANIO YAO BAADA ELIMU ILIYOKUFIKIA,HUTAPATA KUTOKA KWA MWENYEZI MUNGU MLINZI WALA MSAIDIZI"(2:120).
Msiba ulioje Waislaam wamefuata yale waliyokatazwa!Baada ya miaka kadhaa kupita tangu Mtume kufariki,Waislaam wakagawika Makundi Makundi(Madhehebu)!Mpaka leo hii Waislaam waliopewa Uislaam katika Qur'an kupitia Mtume Muhammad(s.a.w) wameugawa Uislaam wao na umekuwa ni Usunni,Ushia,Uanswaar Sunna,Uahmadiyya n.k. na katika hayo makundi kuna makundi mengine madogo madogo ndani yake!
Sasa kuhusiana na mambo kama hayo Mtume aliambiwa na mapema kwamba "HAKIKA WALE WALIYOIGAWA DINI YAO NA WAKAWA MAKUNDI MAKUNDI HUNA UHUSIANO NAO WOWOTE,BILA SHAKA JAMBO LAO HILO LIPO KWA MWENYEZI MUNGU,KISHA ATAWAAMBIA YALE WALIYOKUWA WAKIYATENDA"(6:159).
SOMO LITAENDELEA.....
Lakini kwa sasa,Hebu tujadili kwa pamoja,Ni kitu gani kilichowasababisha Waislaam kuwa na Makundi wakati muongozo wao umekemea waziwazi tena kwa maonyo makali ya Ushirikina na Ukafiri?.Na je,Waislaam wanaweza kurudi katika Uislaam mmoja kama
alouacha Mtume(s.a.w)?

UJUE UISLAAMU HALISI

Assalaam Alaykum,baada ya kuyajua hayo tuliyoyajua kuhusiana na NINI UISLAAM NA NANI NI MUISLAAM,NA NANI SI MUISLAAM.Leo tuendelee na kipengele kingine cha maana ya neno DINI.UISLAAM huliangalia neno Dini kwa maana iliyotofauti na waichukuliayo Wasiokuwa Waislaam!Wasiokuwa Waislaam hulichukulia neno Dini kwa maana ya Imani juu ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu.Kwa mfano katika Katika Kamusi ya Kiingereza ya A.S Horbi with A.B Lowide,A.C Gimson,Oxford Advanced Leaner's Dictionary of current English,Oxford University Press,Nairobi(1962) Ukurasa wa 713,neno Religion(Dini) limefasiriwa hivi "Beliefin the existence of Supernatural ruling power,the Creator and Controller of the universe,Who has given to Man a Spiritual nature which continues to exist after the death of the body"
Tafsiri yake ni kuwa "Dini ni Imani ya kuwepo Mungu Muumba,aliye Muweza na Mwenye Nguvu juu ya kila kitu.Mmiliki wa Ulimwengu ambaye amempa Binaadamu Roho ambayo huendelea kuishi baada ya kifo cha mwili"
Aidha katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu neno Dini limetafsiriwa kama ifuatavyo "Imani inayohusiana na Mambo ya kiroho baina ya Binaadamu na Mwenyezi Mungu,au njia ya kuhusiana na Mwenyezi Mungu".Kwa tafsiri hizi Makafiri wao hudai kuwa hawana Dini kwa kuwa hawana Imani juu ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu.
Lenin mmoja wa wasomi wa Kikafiri anasema "Every body must be absolutely free to profess any Religion he pleases or no Religion whatever,i.e to be a Atheist which every socialist is as a rule...." Tafsiri yake ni kuwa "Kila Mtu hana budi kuwa huru kabisa kufuata Dini yoyote anayoitaka au asiwe na Dini kabisa,yaani awe Kafiri,jambo ambalo inambidi kila mjamaa awe hivyo...."
Neno Dini katika Lugha ya Kiarabu hufasiriwa kama Mila,Utamaduni,Desturi,Njia,Utratibu au Mfumo fulani.Katika Uislaam Neno Dini maana yake ni "Utaratibu au Mfumo wa Maisha ulioanzishwa na Mwenyezi Mungu au Kiumbe".Kwa maana hiyo hakuna Mtu asiyekuwa na Dini kwani ni lazima Mtu awe amefuata utaratibu fulani ambao aidha amejipangia mwenyewe au amepangiwa!
Na kwa mtazamo wa Uislaam Dini(Mifumo ya Maisha) ipo mingi tu,ndio maana Mtume aliambiwa aseme kuwaambia Makafiri kuwa "NYINYI MNA DINI YENU,NA MIMI NINA DINI YANGU"(Sura ya 106 Aya ya 6).Kwa maana nyingine Mtume alikuwa akiwaambia kuwa "NYINYI MNA MFUMO WENU WA MAISHA,NA MIMI NINA MFUMO WANGU WA MAISHA"Tofauti ni kuwa Mfumo aliokuwa akiufuata Mtume umetungwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na Mfumo waliokuwa wakiufuata Makafiri walijitungia wenyewe!
"INNAD DIINA INDALLAAHIL ISLAAM..."Mwenyezi Mungu ananadi kupitia kinywa cha Mtume(s.a.w),yenye Tafsiri kwamba "HAKIKA DINI INAYOKUBALIKA MBELE YA MWENYEZI MUNGU NI UISLAAM"(Sura ya 3 Aya ya 19).Ukiyakunjua zaidi maneno hayo kwa maana ya neno Uislaam na neno Dini tulizokwishaziona ni kuwa "HAKIKA MFUMO WA MAISHA UNAOKUBALIKA MBELE YA MWENYEZI MUNGU NI WAKUTII NA KUNYENYEKEA AMRI,SHERIA NA HUKUMU ZA MWENYEZI MUNGU"
Na kwa kumalizia somo letu kwa Siku ya leo,namalizia kwamba "NA ANAYETAFUTA DINI ISIYOKUWA YA UISLAAM,HAITOKUBALIWA KWAKE.NAYE AKHERA ATAKUWA NI MIONGONI MWA WENYE HASARA"(Sura ya 3 Aya ya 85).Nayo tukiikunjua inakuwa "NA ANAYETAFUTA MFUMO WA MAISHA USIOKUWA WA KUTII NA KUNYENYEKEA AMRI,SHERIA NA HUKUMU ZA MWENYEZI MUNGU,HAUTOKUBALIWA KWAKE.NAYE AKHERA ATAKUWA NI MIONGONI MWA WENYE HASARA"
Shime ndugu zangu tuishi katika Utaratibu na Mfumo aliouridhia Allah!
"SOMO LITAENDELEA INSHAALLAH......."